Jicho ni kiungo ambacho binadamu anapaswa kuwa makini kukilinda maana kuwapo kwake kunasaidia viungo kutenda kazi vyema.
idadi ya wagonjwa wengi wakisukari nchini na duniani inazidi kuongezeka. Ugonjwa huu wa macho huwapata watu wenye
kisukari cha muda mrefu.
Kuwapo kwa ugonjwa wa kisukari husababisha kuharibika kwa retina.
Hii ni sehemu ya nyuma ya jicho
ambayo inaundwa kwa utando wa neva ama mishipa ya fahamu.
Mishipa hii ya fahamu ni muhimu sana katika kumuwezesha mtu
kuona. Ndio inayopokea taswira ya vitu na kuipeleka katika ubongo kwa ajili ya tafsiri.
Kuathirika kwa neva hizi ni tatizo la hatari kwa uwezo wa jicho kuona kwani inaweza kusababisha kuwa na uwezo mdogo wa kutambua taswira ya vitu. Hali hii isipotibiwa
mapema, husababisha ulemavu wa kudumu.
Kisukari ni ugonjwa unaoingilia uwezo wa mwili kutumia na kuhifadhi sukari mwilini. Hii husababisha madhara makubwa mwilini. Sukari ndio nishati inayotegemewa na mwili katika kuendesha shughuli mbalimbali.
Kwa kawaida sukari katika mwili inatakiwa iwe katika kipimo cha saba hadi 12 (7-12).
Uwapo wa sukari nyingi katika
mzunguko wa damu husababisha madhara mbalimbali mwilini ikiwamo sehemu ya jicho ya nyuma
iitwayo retina.
Kadri sukari inavyozidi na muda unavyosogea, mfumo wa mzunguko wa damu katika jicho huathirika.
Ugonjwa hutokea pale sehemu ya retina inapokosa lishe kutoka kwenye vishipa vidogo
vinavyoathirika kutokana na wingi wa sukari mwilini.
Hali hii ikiendelea husababisha mishipa kuvujisha damu na maji maji hivyo kuzifanya tishu za retina
kuvimba na kuwapo na taswira yenye ukungu.
Tatizo hili huathiri macho yote
mawili na kadri mtu anavyoendelea kuugua kisukari ndivyo anavyokua
katika hatari ya kuathirika na
ugonjwa huu zaidi.
Dalili za ugonjwa huu Kuona ukungu au vidoadoa katika taswira unayotazama. Inawezekana pia akaona mawimbi wakati wa kutazama kitu, kushindwa kuona vizuri hasa nyakati za usiku, kuona
giza au kidoa katikati ya taswira imayoonekana.